Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetangula amesitisha zoezi la kuwapiga msasa makatibu walioteuliwa na Rais William Ruto kuhudumu katika wizara mbali mbali kufuatia uamuzi wa mahakama.
Katika barua kwa wenyekiti wa kamati za bunge ambazo zimekuwa zinawapiga msasa makatibu hao, Wetangula amesema zoezi hilo limesitishwa hadi kesi hiyo itakaposkizwa na uamuzi kutolewa.
Hata hivyo Wetangula ameagiza mawakili wa bunge kukata rufaa ya uamuzi huo na kuruhusu zoezi hilo kuendelea.
Jaji Nzioki Makau wa Mahakama ya leba alisitisha kwa muda zoezi hilo kufuatia kesi iliyowasilishwa na chama cha mawakili humu nchini LSK.
Katika kesi hiyo LSK kupitia kwa mawakili wake iliidai kuwa Rais Ruto hakuzingatia sheria katika uteuzi wa makatibu hao.
LSK inadai kuwa usawa wa maeneo na makabila haukuzigatiwa kwani nusu ya makatibu hao wateule wanatoka katika maeneo ya Mlima Kenya na Bonde la Ufa.
Chama hicho cha mawakili pia kimedai kuwa orodha hiyo haijatimiza usawa wa jinsia.
Rais Ruto aliwateua makatibu hao tarehe moja mwezi wa Novemba mwaka wa 2022.