Muungano wa vyama vya wafanyikazi nchini COTU umelaani vikali hatua ya serikali kuongeza bei ya mafuta.

Katika taarifa, katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli anaishtumu serikali kwa kutojali raia wake na badala yake kuwabebesha mzigo wa kulipa ushuru.

Katibu huyo anashangaa iwe je serikali inaagiza mafuta nchini kwa shilingi 49.97 na kuishia kuwauzia wakenya kwa shilingi 134.

Anasema kwa mfano katika taifa jirani la Uganda ambalo halina bandari yake, linauza mafuta kwa bei nafuu ya shilingi 110, ikilinganishwa na Kenya ambayo ina bandari.

Atwoli sasa anamtaka Rais Uhuru Kenyatta kujitokeza mwenyewe na kujieleza mbele ya wakenya la sivyo atarajie migomo kutoka kwa kila kona kwani anadia wafanyikazi wamefinywa na maisha.

Katika mahojiano ya kipekee na kituo hiki, Muungano wa matatu nchini (MOA) unasema vyama vya ushirika viko huru kuongeza nauli baada ya kupandishwa kwa bei ya mafuta.

Katika hatua ambayo itakuwa mzigo zaidi kwa mkenya wa kawaida, mwenyekiti wa muungano huo Simon Kimutai anasema hawana budi ila kuongeza nauli kwani serikali imeshindwa kuwalinda raia wake.

Wakenya katika maeneo mbalimbali nchini nao wanaendelea kulalamikia kupanda kwa bei ya mafuta.

Mjini Migori, shughuli za uchukuzi zimetatizwa baada ya wakaazi kuandamana kupinga kupandishwa kwa bei za mafuta.

Wakaazi hao wamalalama kwamba wanaumia kutokana na hali ngumu ya maisha ilhali serikali inazidi kuwafinya.

Nyongeza hii ya mafuta imezua madhila gani kwa wakenya?

Douglas Omariba ameandaa taarifa ifuatayo kuhusu mahangaiko ya wakenya na kilio chao kwa serikali.