Kenya ilimaliza ya kwanza kwa medali katika mashindano ya dunia ya riadha kwa chipukizi yaliyoandaliwa katika uwanja wa Kasarani jijini Nairobi Jumapili.

Katika siku ya mwisho ya mashindano hayo, Kenya ilijinyakulia medali saba zikiwemo dhahabu tatu, fedha moja na shaba tatu.

Kwa ujumla, Kenya ambaye alikuwa mwenyeji wa mashindano hayo alimaliza ya kwanza duniani kwa kushinda medali 16; dhahabu nane, fedha moja na shaba saba.

Mbali na kutetea taji lake, Kenya imefanya vyema katika mashindano hayo ya chipukizi ikilinganisha na mwaka 2018 nchini Finland ambapo walishinda medali 11.