Maafisa sita wa polisi waliokamatwa kuhusiana na mauaji ya ndugu wawili Kianjokoma kaunti ya Embu watazuiliwa kwa siku 14 zaidi.

Mahakama imeagiza washukiwa hao Benson Mbuthia, Consolata Kariuki, Martin Wanyama, Lilian Cherono, Nicholas Sang na James Mwaniki kuzuiliwa katika kituo cha polisi cha Capitol Hill kuwapa wapelelezi muda wa kumaliza uchunguzi.

Hii ni baada ya mahakama kukubaliana na upande wa mashtaka uliosema kuwa iwapo wataachiliwa, huenda wakahitilafiana na uchunguzi au hata kuwatishia mashahidi.

Washukiwa hao walikuwa kwenye zamu wakati Emmanuel na Benson Ndwiga walikamatwa kwa madai ya kukiuka kafyu kabla ya kifo chao.

Kesi hiyo itatajwa tena tarehe 31 mwezi huu wa Agosti.

Benson na Emmanuel walizikwa siku ya Ijumaa wiki iliyopita kwenye mazishi ambayo yalijawa huzuni na simanzi na wito wa haki kwa familia.