Serikali ya Kenya kwa mara nyingine imeonya shule za umma ambazo zinakiuka mwongozo wa karo uliotolewa na wizara ya Elimu kufuatia lalama kutoka kwa umma.

Katibu katika wizara Elimu Paul Kibet ametishia kuwa walimu wakuu ambao shule zao zitapatikana zikiwatoza wanafunzi karo zaidi ya iliyopendekezwa na serikali watachukuliwa hatua za kinidhamu na pia kushtakiwa.

Katika barua kwa wakurugenzi wa Elimu katika kaunti ambayo meza ya Shajara imeipata, Kibet amewaagiza kufanya uchunguzi wa shule hizo na kupiga ripoti kwao ili hatua zichukuliwe.

Kibet anasema baadhi ya shule zimekuwa zikikata karo ambayo wanafunzi wanalipa kugharamia malipo mengine ambayo hayajaidhinishwa na kisha wanafunzi kutumwa nyumbani kwa kisingizio cha kutomaliza karo.

Wizara ya Elimu sasa inasema hata katika shule ambazo wanafunzi hula chakula cha mchana shuleni, wazazi hawafai kulazimishwa kulipia wanao na kutaka shule kupunguza ada hizo kwani muhula wa masomo pia umepunguzwa.

Shule yeyote ambayo inapania kuwatoza wanafunzi ada zaidi, imetakiwa kuandika barua kwa waziri wa Elimu na kupata idhini rasmi kabla ya kuanza kutekeleza.

Katika mwongozo huo, karo katika shule za kitaifa imepunguzwa kwa shilingi 8,500, huku karo ya shule za ngazi ya kaunti na shule zingine ikipunguzwa kwa shilingi 5,500.

Hii ina maana kuwa wazazi walio na wanafunzi katika shule za kitaifa watalipa shilingi 45,054 huku wazazi walio na wanafunzi katika shule za kaunti na zingine wakitakiwa kulipa shilingi 39,554.