Miili ya ndugu wawili imepatikana katika hifadhi ya hospitali ya Embu Level Five siku tatu baada ya kushikwa na Polisi kwa kudaiwa kuvunja masharti ya kuzuia msambao wa ugonjwa wa corona.

Benson Njiru, 22 na Emmanuel Mutura, 19 walionekana hai mara ya mwisho mjini Kianjokoma Jumapili usiku walipokamatwa na Polisi kwa kupatikana nje saa za kafyuu.

Familia yao inasema wawili hao waliteswa na kisha kuuawa na maafisa wa Polisi.

Hata hivyo mkuu wa Polisi Embu Mashariki Emily Ngaruiya anasema ndugu hao walikufa baada ya kuruka kutoka kwa gari la Polisi lililokuwa linaendeshwa.