Innocent Makokha, mshukiwa wa mauaji ya mpenziwe Christine Ambani, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Kariri amekamatwa na wapelelezi wa idara ya DCI katika eneo la Chokaa, Kayole kaunti ya Nairobi .

Mwili wa Christine,23, mwanafunzi wa mwaka wa tatu ulipatikana katika chumba cha kukodisha Githurai mnamo Julai 13, 2021 ukiwa na majeraha ya visu shingoni.

DCI inasema kabla ya kukutana na mauti yake, Christine alikuwa ameondoka shuleni Mwihoko kukutana na mpenziwe Githurai ambapo walikodesha chumba cha kulala.

Siku hiyo marehemu alikuwa arudi shuleni kwa mtihani mchana lakini Makokha alimshawishi asirejee shuleni na ndio usiku huo akamdunga kisu mara kadhaa kabla ya kuhepa na kwenda mafichoni.

Makokha,23, mwanafunzi wa chuo kikuu cha Mt. Kenya kisha alichukua simu ya Christine na kuitisha Sh87,000 kutoka kwa familia yake.

Uchunguzi zaidi wa DCI umebaini kuwa Makokha amehusishwa na mauji kama hayo awali ila maswali yameibuka kuhusu alivyokwepa mkono wa sheria.

Rekodi yake ya uhalifu inaonesha kuwa alikamatwa Februari 2, mwaka huu wa 2021 kwa mauaji ya nduguye, shemejiye na mwanao wa umri wa mwaka mmoja baada ya kuteketeza nyumba yao.

Makokha atafikishwa mahakamani kushtakiwa kwa mauaji.