Mwanamke mmoja amewaua kwa kuwanyonga wanawe wawili kabla ya kujisalimisha kwa maafisa wa polisi katika eneo la Dagorreti kaunti ya Nairobi.

Diana Nasimiyu anaripotiwa kuwaua Sydney Miheso na Miracle Miheso wenye umri wa miaka minne na miwili mtawalia kabla ya kujipeleka katika kituo cha polisi cha Waithaka.

Ripoti ya polisi inaonyesha kuwa mwanamke huyo alifika kituoni mwendo wa saa moja usiku hapo jana Jumapili na kujishtaki.

Polisi walipoenda nyumbani kwa mshukiwa, walipata miili ya wawili hao ikiwa imelazwa kwa kiti cha sofa.

Duru zaarifu kuwa Diana na mumewe wamekuwa wakigombana hali iliyosababisha mama mkwe kusafiri kutoka Lugari kuja kuwasaidia kutatua ugomvi wao.

Uchunguzi umeanzishwa kubaini kiini cha mwanamke huyo kuua watoto wake.