Watu wachache pekee ndio walifaulu kupata msaada wa kifedha kutoka kwa serikali kwenye mpango uliolenga kuwafikia watu wasiojiweza katika jamii kipindi cha corona imesema ripoti ya Human Rights Watch (HRW).

Ripoti hiyo enye kurasa sitini na sita inaonesha kwamba hakukuwa na uwazi kwenye utoaji wa pesa hizo huku ukabila na mapendeleo yakihesheni kwa waliosimamia mpango huo.

Mkurugenzi wa shirika hilo kanda ya Afrika Mashariki Otsieno Namwaya anasema serikali ilikosa kuweka mikakati kabambe kuhakikisha kwamba walengwa wamefikiwa na hivyo kuwaachia watu wachache kutumia fursa hiyo kujinufaisha.

Katika mapendekezo yake, HRW inataka asasi za uchunguzi kuanzisha uchunguzi na kuwaadhibu waliohusika na sakata hiyo.

Takriban watu 136 walihojiwa na shirika hilo kati ya Julai 2020 na Februari mwaka huu wa 2021 wengi wao wakiwa maafisa wa serikali na wakaazi wa mitaa duni jijini Nairobi.