Agosti 20,2021 saa tatu asubuhi itakuwa ndio siku na saa ambapo mahakama ya rufaa itatoa uamuzi wake kuhusu rufaa iliyowasilishwa kupinga uamuzi wa mahakama kuu uliosimamisha ubadilishaji wa katiba katiba kupitia mchakato wa BBI.
Rais wa mahakama hiyo Daniel Musinga amesema haya baada ya kukamilika kwa vikao vya kusikiliza rufaa hiyo ambapo imekuwa ni hali ya kila mwamba ngoma huvutia kwake.
Imekuwa ni hali ya kila mwamba ngoma huvutia kwake kwenye siku ya mwisho ya vikao vya kusikiliza rufaa inayopinga uamuzi wa mahakama kuu uliosimamisha marekebisho ya katiba kupitia BBI.
Wakosoaji wa mchakato huo wamelitaka jopo la majaji saba wa mahakama ya rufaa likiongozwa rais Daniel Musinga kukubaliana na uamuzi huo huku walalamishi wakiongozwa na rais Uhuru Kenyatta pamoja na kinara wa chama cha ODM Raila Odinga wakitaka uamuzi huo kubatilishwa.
Kwenye vikao vya mwisho, mkenya mmoja anayepinga BBI sasa anaitaka mahakama ya rufaa kumshurutisha Rais Uhuru Kenyatta kulipa pesa za mlipa ushuru zilizotumika kufadhili mchakato wa BBI.
Kupitia kwa wake Christian Andole, mkenya huyo Morara Omoke anasema mahakama kuu ilikosea wakati haikumshurutisha Uhuru kuwalipa wakenya pesa zao alizotumia katika mchakato ambao umeutaja kuwa kinyume cha sheria.
Wakili John Khaminwa anayewakilisha tume ya kutetea haki za kibinadamu KHRC ameliambia jopo hilo kwamba hawafai kumsikiliza Rais Uhuru Kenyatta kwa sababu hapendi kuheshimu mahakama.
Msimamo wake umeungwa mkono na wakili Martha Karua anayehoji kwamba huenda mabadiliko ya katiba kupitia kwa mswada wa BBI ni njama ya wanasiasa kutaka kusalia uongozini.
Lakini, rais Uhuru Kenyatta alipoteza lini haki zake kama raia wa Kenya? Ndilo la mawakili wa Uhuru ambao wameiambia mahakama kwamba mteja wao hakupewa stakabadhi zinazoonesha kwamba alishtakiwa kwa kukiuka katiba alipohusika na mchakato wa BBI.
Mawakili wa Raila Odinga wakiongozwa na James Orengo wanashikilia kwamba mchakato mzima wa BBI ulizingatia vigezo vyote vya kisheria.