Chama cha ODM kinachoongozwa na Raila Odinga kimeondoa ada ya Sh100 inayotozwa wanaotaka kusajiliwa kuwa wanachama wapya wa chama hicho kwa muda wa miezi mitatu ijayo.

Katibu mkuu wa chama hicho Edwin Sifuna katika taarifa amesema hatua hii imechukuliwa baada ya watu wengi kulalamikia hali ngumu ya uchumi inayosababishwa na janga la corona.

Sifuna ameeleza kwamba chama hicho kimekuwa kikiendesha shughuli ya kuwasajili wanachama wapya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022 zoezi analosema limeshuhudia kuongezeka kwa idadi ya wanachama wake.

Ametoa wito kwa wafuasi wa chama hicho cha Chungwa kutumia fursa hiyo ya miezi mitatu kujisajili ili kuwawezesha kushiriki kwenye uchaguzi wa mashinani na mchujo unaokuja.