Mahakama ya Rufaa imeanza kusikiliza kesi inayopinga uamuzi wa mahakama kuu uliosimamisha marekebisho ya katiba kupitia mchakato wa BBI.

Mwanasheria mkuu Kihara Kariuki kupitia kwa wakili wa serikali Kennedy Ogeto amelitaka jopo linalosikilzia rufaa hiyo chini ya uongozi wake rais wa mahakama ya rufaa Daniel Musinga kubatilisha uamuzi huo wa mahakama kuu kwa misingi kwamba ulienda kinyume na katiba na matamanio ya wananchi kutaka kubadilisha katiba.

Ameiambia mahakama hiyo kwamba majaji wa mahakama kuu wakiongozwa Joel Ngugi walichukulia suala hilo kuwa la kibinafsi, kiasi kwamba wakaidhinisha kushtakiwa kwa Rais Uhuru Kenyatta.

Ogeto anasema wanachowaomba majaji hao akiwemo Roselyne Nambuye, Hannah Okwengu, Patrick Kiage, Gatembu Kairu, Fatuma Sichale na Francis Tuyoitt ni kushikilia katiba ya Kenya.

Walalamishi wengine kwenye kesi hiyo ni rais Uhuru Kenyatta, kiongozi wa chama cha ODM Raila Odinga na tume ya uchaguzi na mipaka IEBC.