Ilikuwa ni vifijo, nderemo, sifa na Utukufu kwa Mungu katika mtaa mmoja huko Pipeline wakati maafisa kutoka idara ya DCI walirejesha nyumbani mtoto wa miaka tatu aliyetekwa nyara mapema wiki iliyopita.

Wazazi wa mtoto huyo Michelle Kemunto hawakuficha furaha hiyo, huku majirani na marafiki wakiungana nao kusherehekea na kutoa shukrani kwa Mungu kwa kumwona tena mtoto wao akiwa hai baada ya siku tisa za mahangaiko.

Maafisa wa DCI wanasema mtoto huyo alitekwa nyara na watu wasiojulikana nje ya nyumba yao wakati akicheza na rafikiye huku wazazi wake wakiwa shughuli zao za kawaida.

Mtekaji nyara ambaye anaaminika kuwa mwanamke wa makamo alimuacha mtoot huyo kwa msamaria mwema mmoja na kumtaka amchungie afike mtaani Tassia kwa shughuli kabla ya kurejea kumchukua.

Hata hivyo siku tatu baadae, mama huyo alimpigia msmaria mwema simu na kumhadaa kuwa alikuwa amepata ajali, sababu ambayo ilisababisha yeye kutorudia mtoto huyo aliyedai ni wake.

Alimtaka msamaria mwema huyo kupeana mtoto huyo kwa mtu mwingine ambaye alikuwa anatuma kumchukua.

Hata hivyo msamaria mwema huyo alishuku kilichokuwa kikiendelea, alipiga ripoti kwa kituo cha polisi cha Tassia na uchunguzi kubaini kuwa mtoto huyo alikuwa ametekwa nyara, na hiyo ilikuwa njama ya kumficha.