Serikali imetangaza masharti mapya kwenye kaunti 13 za Nyanza na Magharibi ambazo zimetajwa kama ‘HATARI’ kwa msambao wa virusi vya corona.

Kafyuu kwenye kaunti za Busia, Vihiga, Kisii, Nyamira, Kakamega, Kericho, Bomet, Bungoma, Trans-Nzoia, Kisumu, Siaya, Homa-Bay & Migori itaanza kuanzia saa moja jioni hadi saa kumi alfajiri.

Waziri wa afya Mutahi Kagwe ametangaza kuwa masharti hayo yataanza kutekelezwa rasmi kuanzia Ijumaa (Juni 18).

Kwenye mipaka, madereva watahitajika kuwa na vyeti vinavyoonesha kwamba hawana corona huku masoko yenye shughuli nyingi yakifungwa kwa siku 30 zijazo.

Mikutano yote ya umma katika kaunti hizo imepigwa marufuku ikiwemo sherehe za nyumbani na michezo.

Mazishi ni sharti yafanyike saa 72 baada ya mtu kufariki.

Wakati uo huo

Kenya imedhibitisha maambukizi mapya 660 ya corona baada ya kupima sampuli 6,176 katika muda wa saa Ishirini na nne zilizopita.

Idadi ya visa vya ugonjwa huo nchini kwa sasa ni 177,282 huku kiwango cha maambukizi kikiwa asilimia 10.7%.

Habari njema ni kwamba wagonjwa 812 wamepona na kufikisha idadi hiyo kuwa 122,018 huku SITA zaidi wakifariki na kufikisha idadi hiyo 3,434.

Wagonjwa waliolazwa hospitalini ni 1,059 huku wanaoshughulikiwa nyumbani wakiwa 4,812.