Mahakama imetoa agizo linalozuia kuchunguzwa na kushtakiwa kwa majaji sita ambao rais Uhuru Kenyatta alikataa kuwaapisha.

Jaji wa mahakama kuu James Makau ameamuru kwamba hakutakuwa na mapendekezo yoyote yatakayotolewa kuhusu kuondolewa kwao.

Mahakama hiyo aidha imemzuia rais dhidi ya kuweka wazi ripoti ya kijasusi iliyotilia shaka maadili majaji hao.

Majaji hao ni Aggrey Muchelule, George Odunga, Weldon Korir na Joel Ngugi waliokuwa wahudumu kwenye mahakama ya rufaa.

Hakimu Mkuu Evans Makori na msajili wa mahakama kuu Judith Omange vile vile hawakuapishwa.

Mahakama imetoa uamuzi huo baada ya mlalamishi Benard Okello kuiambia mahakama kwamba rais Kenyatta aliwabagua majaji hao ilhali katiba inamshurutisha kuwaapisha baada ya kupokea orodha kutoka kwa tume ya huduma za mahakama JSC.