Mamlaka inayosimamia Nairobi (NMS) inatazamiwa kufanyia majaribio ya tatu stendi ya matatu ya Green Park Jumatano ijayo.

Majaribio hayo yanatazamiwa kuendeshwa kati ya saa kumi na mbili na saa mbili asubuhi.

Matatu zinazohudumu kwenye barabara za Langata, Ngong, Rongai, Kibra, Kawangware, Kikuyu, Highrise, Ngumo, Kiserian, Otiende, Madaraka na Nairobi West zitashirikishwa kwenye majaribio hayo.

Aidha, matatu zinazohudumu katika eneo la Moi Avenue nje ya Development, AGHRO na Gill house, Hataki, Ambassador, Mfangano, Kencom na kituo cha Railways vile vile zitahusishwa.

Majaribio hayo yatajumuisha kushusha na kubeba abiria katika kile mkurugenzi wa NMS Mohammed Badi anasema ni kuwawezesha wahandisi kuunda mbinu itakayotumika kupunguza msongamano wa magari katikati mwa jiji.