Serikali ya kaunti ya Laikipia imekubali kubeba mzigo baada ya wagonjwa wawili kufariki kutokana na utepetevu wa Wauguzi kwenye hospitali ya rufaa ya Nanyuki.

Katika taarifa, waziri wa afya wa kaunti hiyo Rose Maitai amesema wahudumu wawili wa afya waliokuwa kwenye zamu siku hiyo wamesimamisha kazi huku uchunguzi zaidi ukiendelea.

Maafisa wa afya waliosimamishwa kazi baada ya uchunguzi wa mwanzo ni Phydelis Nabwoba na Clement Kimani.

Kaunti hiyo vile vile imeialika idara ya upelelezi DCI kuingilia kati na kufanya uchunguzi zaidi kwa makusudi ya kuwachukulia hatua za kisheria wahusika.

Madiwani wa kaunti hiyo wamefika katika hospitali hiyo ya Nanyuki wakitaka hatua zaidi kuchukuliwa.

Hii ni baada ya familia moja kulalalama kuwa mpendwa wao alifariki akisubiri matibabu wakati wauguzi walikuwa wakisherehekea siku ya kuzaliwa kwa mmoja wao.

Familia nyingine pia inalalama kuwa mpendwa wao alifariki baada ya wauguzi kuwatuhumu kuwa na kiburi na hivyo kukataa kushughulikia mgonjwa wao.