Shirika la wanasheria wa kimataifa (ICJ) tawi la Kenya limemtaka rais Uhuru Kenyatta kukoma kutoa matamshi yanayohujumu uhuru wa idara ya mahakama.

Katika taarifa, ICJ imeshauri rais Kenyatta kuwa na subira licha ya kutoridhika na uamuzi wa mahakama kuu uliosimamisha marekebisho ya katiba kupitia BBI.

Kupitia kwa mwenyekiti wake Kelvin Mogeni, shirika hilo linasema matamshi ya rais Kenyatta wakati wa maadhimisho ya Madaraka Dei mjini Kisumu ilikuwa ni vitisho vya moja kwa moja kwa majaji.

Wamewataka majaji na mahakimu wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Koome na tume ya huduma za mahakama JSC kusalia imara na wasikubali kutishwa na yoyote katika kuwajibikia majukumu yao.

Wakati uo huo

Vuguvugu la Linda Katiba limemsuta vikali rais Uhuru Kenyatta kutokana na kile limetaja kama kuitisha idara ya mahakama.

Katika taarifa, Linda Katiba linahoji kwamba matamshi ya rais Kenyatta wakati wa sherehe za Madaraka Dei mjini Kisumu yaliyoelekezwa kwa idara ya mahakama ni ukiukaji wa sheria na yanaingilia uhuru wa idara hiyo.

Kwa mujibu wa vuguvugu hilo, matamshi ya rais sawa na viongozi wengine yanaunda dhana kwamba mahakama iNawajibikia majukumu yake kwa mapendeleo.