Maafisa wawili wa polisi waliopatikana na hatia ya kumuua kwa kumpiga risasi mwanamke mmoja katika bustani ya City, Nairobi wamehukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani.

Wawili hao waliofutwa kazi William Chirchir na Godfrey Kirui watatumikia kifungo cha miaka saba kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kumuua Janet Wangui asubuhi ya tarehe 20, mwezi wa tano mwaka 2018.

Katika hukumu yake, jaji Stella Mutuku amesema kifungo hicho ni funzo kwa maafisa wengine ambao wanapania kutumia vibaya mamlaka yao.

Polisi hao walimuua kwa kumpiga risasi mwanamke huyo aliyekuwa kwenye gari na binamuye Benard Chege.

Jaji ameamuru kuwa polisi hao walitumia nguvu kupita kiasi ilhali mwanamke huyo hakuwa tishio kwa usalama wao.