Serikali imepokea pigo jingine kutoka kwa idara ya mahakama baada ya jopo la majaji watatu kuharamisha teuzi za watu 128 katika mashirika mbalimbali mwaka 2018.

Katika uamuzi wao, majaji Jessie Lessit, Chacha Mwita na Lucy Njuguna wameamuru kuwa teuzi hizo zilizofanywa na Rais Uhuru Kenyatta na mawaziri wengine zilikiuka katiba.

Majaji hao wameharamisha tangazo la serikali kuwateua watu hao akiwemo aliyekuwa mkuu wa majeshi jenerali Julius Karangi, aliyekuwa Gavana Benjamin Cheboi na Margaret Saitoti.

Kwenye kesi hiyo, mashirika yasiyo ya kiserikali ya Katiba Institute na Africog yalilalama kuwa Rais Kenyatta na mawaziri walikiuka katiba kwa kuwateua wakenya hao bila nafasi hizo kutangazwa kuwa wazi.

Hili ni pigo la karibuni zaidi kwa serikali kutoka kwa mahakama ambayo iliharamisha nafasi za makatibu waandamizi CAS, kuharamisha mawaziri walioteuliwa kuhudumu bila kupigwa msasa na karibuni zaidi kuharamisha mchakato wa BBI.