Baba, mama na mwanao wa kiume wanatazamiwa kufikishwa mahakamani hii leo kwa tuhuma za kumuua binti yao mwenye umri wa miaka kumi na tano.

Watatu hao Frankline Ntwiga, mkewe Benedetta Mbeni na mtoto wao wa kiume Ian Marangu Ntwiga wanatuhumiwa kumuua mwanafunzi huyo wa shule ya wasichana ya Kiteta kaunti ya Makueni kwa madai ya kutoroka nyumbani.

Katika taarifa, idara ya upelelezi nchini DCI inasema baba mtoto huyo alimpelaka katika hospitali ya Coptic usiku wa Alhamisi wiki iliyopita kufanyiwa ukaguzi wa kimatibabu ambao ulionyesha alikuwa mzima.

Hata hivyo walipofika nyumbani, watatu hao walimwangukia kwa kichapo kutumia kipande cha mfereji na walipoona amezirai wakamkimbiza tena katika hospitali hiyo ila alikuwa tayari ashakata roho.

Madaktari wanasema mwili wa msichana huyo ulikuwa na majeraha kila mahali ishara kuwa alikuwa amedhulumiwa.

Mwili wa msichana huyo pia utafanyiwa upasuaji leo kubaini chanzo cha kifo chake anavyoeleza OCPD wa Kilimani Andrew Mbogo.