Tume ya uchaguzi nchini IEBC inatazamiwa kurejelea zoezi la kuhesabu kura katika uchaguzi mdogo wa Juja uliofanyika jana.

IEBC ilisitisha zoezi hilo jana usiku baada ya kuibuka kwa vurugu katika kituo cha kuhesabu kura katika shule ya upili ya Mangu.

Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati anamshtumu Gavana wa Kiambu James Nyoro kwa kuongoza kundi la wahuni kuvuruga zoezi hilo.

Chebukati amewaondolea lawama maafisa wake, na kusema jukumu la kudumisha usalama linasalia na idara ya polisi.

Hata hivyo Chebukati anatoa hakikisho kuwa kura zilizopigwa jana zimelindwa na kwamba zoezi la kuhesabu litarejelewa pindi hali itatulia.

Maafisa wa polisi walilazimika kuingilia kati na kutuliza ghasia jana usiku baada ya vurugu hizo na kuwafurusha wanasiasa waliokuwa wanazua vurugu.

Upande uliokuwa unaongozwa na Gavana Nyoro ulikuwa unalalamikia madai ya wizi wa kura.