Serikali inatazamiwa kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa mahakama kuu uliosimamisha ubadilishaji wa katiba kupitia mchakato wa BBI.

Jopo la majaji watano Joel Ngugi, George Odunga, Jairus Ngaah, Teresia Matheka na Chacha Mwita limeamuru kwamba mchakato huo unakiuka katiba na kwamba rais hana mamlaka ya kuanzisha ubadilishaji wa katiba na badala yake kuhoji kuwa ni mkenya wa kawaida ndiye aliye na uwezo huo.

Majaji hao waliamuru kwamba tume ya uchaguzi na mipaka IEBC haijabuniwa kisheria kusimamia kura ya maamuzi na kwamba Wakenya hawakuhusishwa kikamilifu kupitia kutolewa kwa elimu kwa umma kuhusu BBI.

Kwa mujibu wa majaji hao; vigezo vikuu vilivyosababisha kusimamishwa kwa mchakato huo ni pamoja na;

Rais Uhuru Kenyatta alikosea na kuzidi mamlaka yake alipoanzisha mchakato wa kurekebisha katiba kinyume cha sheria

Kamati iliyoundwa na rais kuongoza mchakato huo inahudumu kinyume cha katiba.

Tume ya uchaguzi na mipaka IEBC haijabuniwa kisheria kusimamia kura ya maamuzi kwa kukosa makamishna wote.

Umma haukuhusishwa kikamilifu kupitia kutolewa kwa elimu kwa umma, kusoma na kuielewa ripoti ya BBI ambao ilipaswa kupewa kila mmoja.

Ni tume ya uchaguzi IEBC pekee ndiyo iliyo na jukumu la kuratibu na kutathmini maeneo bunge mapya.

Rais Uhuru Kenyatta alikaidi sehemu ya SITA ya katiba kwa kuunga mkono na kuanzisha mchakato wa kubadilisha katiba na hivyo kutoa nafasi ya kushtakiwa kwake.

Rais alishindwa kulinda katiba aliyoapa kuilinda alipoapishwa.

Hakuna sheria inayosimamia kuandaliwa kwa kura ya maamuzi

Bunge halina mamlaka ya kubadilisha baadhi ya vipengee kwenye katiba.