Mkuu wa idara ya upelelezi katika eneo la Embakasi, Nairobi Simon Mutia Mwongela amekamatwa kwa kudaiwa kumpiga risasi na kumuua bawabu Kayole.

Inaarifiwa kuwa Mwongela alimpiga risasi mlinzi huyo baada ya kuibuka mzozo baina yao katika eneo moja la burudani.

Walioshuhudiwa tukio hilo wamewaambia Polisi kwamba Mwongela alifika katika eneo hilo mwendo wa saa kumi alfajiri na kuiagiza afunguliwe lango ili alale.

Hata hivyo alipokatazwa na bawabu huyo aliyemfahamisha kwamba muda wa kulala ulikuwa umekwisha, Mwongela alitoa bunduki yake na kuupiga mlango huo risasi ili ufunguke kwa lazima.

Risasi hilo lilienda moja kwa moja na kumfika mlinzi huyo wa usiku ambapo lililomuingia kifuani na kumuua papo hapo.

Kukamatwa kwake kunafuatia agizo la Inspekta mkuu wa Polisi Hillary Mutyambai.

Kwingineko

Maafisa wa usalama Gilgil walimuua kwa kumpiga risasi afisa wa zamani wa Polisi Arnold Madete aliyekuwa anajaribu kukata chuma cha bango ili auze.

Awali, marehemu alikuwa amekutwa na hatia ya kuuza vyuma na alikuwa anahudumia kifungo cha nje.