Idara ya upelelezi nchini DCI imewaonya wakaazi wa Nairobi kujitadhari na genge ambalo limekuwa likiwalaghai watu pesa katikati mwa jiji la Nairobi.

Katika taarifa, DCI inasema genge hilo ambalo linawajumuisha wanaume na wanawake limekuwa likijidai kuwa maajenti wa kampuni moja ya mawasiliano kabla ya kuwalaghai wahasiriwa.

Genge hilo ambalo limekuwa likihudumu katika barabara ya Tom Mboya, karibu na makavazi ya taifa na pia karibu na kituo cha magari cha Railways, linawahadaa wakenya kuwa watapata simu na bidhaa zingine za kielektroniki kwa bei nafuu, kabla ya kuwaibia pesa.

Washukiwa pia wamekuwa wakiwahadaa wapita njia kuwa wanaweza kuwasaidia kutengeneza simu zao, na badala yake wanadukua nambari za siri za M-Pesa kabla ya kuwaibia pesa.

DCI inawataka wakenya ambao wamelaghaiwa na genge hilo kupiga ripoti kwao ili hatua za kisheria zichukuliwe.

Idara hiyo inasema washukiwa hao walikamatwa mbeleni kufuatia ripoti kutoka kwa wananchi waliolaghaiwa lakini wakaachiliwa kwa ukosefu wa ushahidi kwani waliolaghaiwa hawakujitokeza kutoa ushahidi.