Sasa ni rasmi kuwa matokeo ya mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne KCSE yanatolewa hii leo.
Waziri wa Elimu Profesa George Magoha anatazamiwa kutangaza matokeo ya mtihani huo kutoka jumba la Mitihani, barabara ya Dennis Pritt muda wowote kuanzia saa sita na nusu.
Zoezi la usahihishaji lilikamilika siku ya Ijumaa ambapo wanafunzi 751,150 walijisajili kuukalia.
Muda mfupi uliopita, matokeo ya mtihani huo yaliwasilishwa kwa Rais Uhuru Kenyatta katika ikulu ya Rais, Nairobi.
Waziri Magoha alimfahamisha Rais Kenyatta kuhusu matokeo hayo akiandamana na mkuu wa utumishi wa umma Jospeh Kinyua, katibu katika wizara ya Elimu Julius Jwan, afisa mkuu mtendaji wa tume ya huduma za walimu TSC Nancy Macharia na mwenzake wa baraza la mitihani nchini KNEC Mercy Karogo.
Rais Kenyatta amewapongeza watahiniwa wote kwa kujikakamua kuandikisha matokeo bora licha ya hali ngumu kimasomo iliyosababishwa na janga la corona.