Kenya na Uingereza wamefanya mazungumzo yaliyojikita katika kushirikiana kuafikia malengo yenye umuhimu baina ya mataifa hayo mawili.

Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson wamezungumza kwa njia ya simu ambapo wameahidi kushirikiana kupambana na janga la corona.

Ikumbukwe kwamba Uingereza ni miongoni mwa mataifa ambayo yametangulia kutuma msaada wa vifaa vya matibabu nchini India kufuatia wimbi la pili la corona ambalo limesababisha maafa.

Wawili hao vile vile wamejadiliana kuhusu mabadiliko ya tabia nchi sawa na usalama na amani katika kanda hii.

Mazungumzo hayo aidha yameangazia kongamano lijalo la elimu litaloandaliwa kwa ushirikiano wa Kenya na Uingereza.

Kongamano hilo la mwezi Julai linalenga kuhakikisha kuwa wanafunzi wapatao Milioni 175 kote duniani wameenda shuleni.

Kuhusu hali tete ya kisiasa nchini Somalia, wawili hao wameelezea wasiwasi wao kuhusu joto la kisiasa linalozidi kushuhudiwa katika taifa hilo na kuahidi kutumia ushawishi wao kwenye baraza la usalama la umoja wa mataifa na Commonwealth kutanzua mgogoro huo.