Tume ya huduma za mahakama (JSC) sasa iko huru kupendekeza jina la Jaji Mkuu mpya baada ya kukamilisha mahojiano siku ya Ijumaa.

Hii ni baada ya mahakama ya rufaa kusitisha kwa muda utekelezaji wa agizo la mahakama kuu lililozuia tume hiyo kuendelea mbele na mchakato wa kumtafuta jaji mkuu mpya.

Jopo la majaji watatu, Roselyn Nambuye, Patrick Kiage na Sankale Ole Kantai limeruhusu pia tume ya JSC kuendelea mbele na mahojiano ya kumtafuta jaji wa mahakama ya upeo kuchukua nafasi yake Jackton Ojwang aliyestaafu.

Waliohojiwa kumrithi David Maraga aliyestaafu ni Rais wa mahakama ya rufaa William Ouko, majaji Martha Koome, Juma Chitembwe, David Marete, mawakili Fred Ngatia na Philip Murgor pamoja na wasomi wa maswala ya kisheria Profesa Kameri Mbote na Dr. Dr. Moni Wekesa.

Wanaowania wadhifa wa jaji wa mahakama ya upeo kuchukua nafasi ya Jacktone Ojwang’ aliyestaafu ni; majaji Said Chitembwe, Martha Koome, M’inoti Kathurima, Nduma Nderi, William Ouko, Marete Njagi, Joseph Sergon na mawakili Lumumba Nyaberi na Alice Yano.