Mashirika ya kijamii yanamtaka Mwanasheria Mkuu Paul Kihara kujiuzulu kwa kushindwa kumshauri Rsais ipasavyo kuhusu uteuzi wa makatibu wasaidizi (CAS).

Wito huu unajiri siku chache baada ya mahakama kuu kuamuru kuwa makatibu hao wasaidizi wako afisini kinyume cha sheria na kwamba uteuzi wao ulikiuka katiba.

Mashirika hayo kupitia kwa mwenyekiti wake Suba Churchill yanahoji kwamba mwanasheria mkuu ndiye mshauri mkuu wa serikali katika maswala mbalimbali ya kisheria na hivyo kushangaa iweje Paul Kihara alishindwa kumpa Rais Uhuru Kenyatta ushauri unaofaa kuhusu uteuzi wa makatibu wasaidizi.

Kwa mujibu wa mashirika hayo, serikali imekuwa ikijipata pabaya kuhusu maswala yanayoambatana na sheria tangu kuteuliwa kwa Kihara kwa wadhifa wa Mwanasheria Mkuu.

Wanamtuhumu Kihara kutokana na kile wanataja kama kushindwa kulinda na kuitetea katiba ambayo aliapa kuilinda alipokula kiapo kabla ya kuanza rasmi majukumu yake.

Katika uamuzi wake kwenye kesi iliyowasilishwa mahakamani na mwanaharakati Okiya Omtatah, jaji wa mahakama kuu Anthony Mrima pia aliamuru kuwa mawaziri walioteuliwa na Rais aliposhinda muhula wa pili walifaa kuidhinishwa na bunge la kitaifa.

Aidha, jaji huyo ameamuru kuwa makatibu wakuu ambao hawakuorodheshwa, kuhojiwa au kuteuliwa kulingana na sheria wako afisini kinyume cha sheria.

Hata hivyo jaji huyo alizuia utekelezwaji wa uamuzi huo kwa sababu taifa bado linapambana na janga la corona.