Tume ya huduma za mahakama (JSC) imesema itangoja idhini ya mahakama kabla ya kuendelea mbele na kibarua cha kutangaza jina la atayejaza wadhifa wa Jaji Mkuu.

Mwenyekiti wa tume hiyo Olive Mugenda vile amesema mahojiano ya kumtafuta jaji wa mahakama ya upeo yaliyokuwa yaanze wiki ijayo yamesitishwa wakisubiri uamuzi wa mahakama utakaotolewa wiki ijayo.

Itakumbukwa kwamba majaji watatu wa mahakama kuu Anthony Mrima, Reuben Nyakundi na Wilfrida Okwany walitoa maagizo ya muda kuzuia mchakao wa kumtaja jaji mkuu sawa kumtafuta jaji wa mahakama ya juu zaidi nchini kufuatia kesi iliyowasilishwa mahakamani.

Mahojiano ya kujaza wadhifa wa Jaji Mkuu kufuatia kustaafu kwa David Maraga yamekamilika rasmi huku watu 10 wakiwemo majaji, mawakili na wasomi wa maswala ya kisheria wakihojiwa.

JSC mnamo Jumatatu ijayo ilikuwa imeratibiwa kuendesha mahojiano ya kumtafuta jaji wa mahakama ya upeo kufuatia kustaafu kwa jaji Jackton Ojwang.