Shughuli ya kumtafuta Jaji Mkuu mpya imeingiwa na shaka baada ya mahakama kuu kutoa agizo linaloizuia tume ya huduma za mahakama (JSC) dhidi ya kuendelea na mahojiano ya kumsaka mrithi wa David Maraga aliyestaafu.

Katika uamuzi wao, majaji wa mahakama kuu Anthony Mrima, Reuben Nyakundi na Wilfrida Okwany wameiruhusu JSC kuendelea na mahojiano hayo ila wasitoe mapendekezo kuhusu atakayejaza wadhifa huo.

Majaji hao aidha wameizuia JSC dhidi ya kuendesha mahojiano ya kumtafuta jaji wa mahakama ya upeo kujaza nafasi ya Jacktone Ojwang aliyestaafu hadi kesi iliyowasilishwa mahakamani itakaposikilizwa na kuamuliwa.

Watatu hao wamesitisha mchakato huo kwa msingi kwamba kesi iliyowasilishwa mahakamani na walalamishi Philip Muchiri, Damaris Ndirangu na Memba Ocharo inaibua maswala yenye uzito wa kikatiba.

Walalamishi wanahoji kuwa baadhi ya wanaowania wadhifa wa Jaji Mkuu hawajatangaza wazi mali yao kwa umma kulingana na katiba na pia wanapinga jopo linaloendesha mahojiano hayo kuongozwa na Olive Mugenda akisema kwa mujibu wa sheria, naibu jaji mkuu Philomena Mwilu ndiye anapaswa kuwa mwenyekiti.