Kenya na DR Congo wametia saini mikataba minne ya ushirikiano kwenye sekta mbalimbali ikiwemo usalama, uchukuzi na uchumi.

Miongoni mwa mikataba hiyo iliyosainiwa na rais Uhuru Kenyatta pamoja na mwenyeji wake Felix Tshisekedi ni ushirikiano wa jumla kuendeleza biashara na kubuni nafasi zaidi za kazi.

Mikataba hiyo ya uchumi inaangazia kilimo, elimu, afya, michezo na utalii.

Kuhusu usalama, Kenya na DRC wamekubaliana kushirikiana kupambana na ugaidi, uhamiaji, kupambana na uhalifu wa kimtandao sawa na kuboresha usalama kwenye mipaka yao.

Rais Uhuru Kenyatta akizungumza wakati wa kutiwa saini kwa mikataba hiyo amesema huu ndio mwanzo wa kuimarisha uhusiano wa karibu baina ya mataifa haya mawili.