Wakili Philip Kipchirchir Murgor amekataa kujibu baadhi ya maswali aliyokuwa anaulizwa na tume ya huduma za mahakama (JSC) kuhusu wadhifa wa jaji mkuu.

Wakili huyo amekataa kutoa mtazamo wake kwenye maswala yenye uzito wa kikatiba ikiwemo kushtakiwa kwa rais na naibu wake iwapo atateuliwa kuwa jaji mkuu.

Wakili Murgor ameielezea JSC kwamba ana uzoefu wa kutosha kuwa jaji mkuu haswaa ikizingatiwa kwamba ameshughulikia kesi mbalimbali kama vile sakata ya Goldenberg.

Murgor alikuwa wakili wa serikali katika afisi ya mwanasheria mkuu kati ya mwaka 1986 na 1992 na kisha aliteuliwa kuwa mwendesha mkuu wa mashtaka ya umma mwaka 2003.

Wakili Murgor ni mzaliwa wa mwaka 1961 katika kaunti ya Elgeyo Marakwet na ana uzoefu wa miaka 34 katika taaluma ya uanasheria.

Wakili Murgor anahojiwa siku moja baada ya jaji David Marete Njagi kufika mbele ya JSC kunadi sera zake ambapo aliahidi kuweka mikakati kabambe kupambana na ufisadi katika idara ya mahakama.

Wengine ambao wamehojiwa kwa wadhifa huo ni; Said Juma Chitembwe, Profesa Patricia Kameri Mbote na Martha Koome Karambu.