Afisa wa GSU Hudson Wakise na mkewe ambaye ni Polisi wa trafiki Kilimani Pauline Wakasa walifariki kwa sababu ya kuvuja damu nyingi.

Matokeo ya upasuaji yanaonesha kuwa wawili hao ambao ni mtu na mkewe walipoteza damu nyingi kutokana na majeraha ya risasi.

Wakise aliyekuwa mmoja wa walinzi wa waziri wa usalama wa ndani Dkt. Fred Matiang’i alimuua kwa kumpiga mkewe risasi kabla ya kujiua kwa kujipiga risasi kufuatia mzozo wa kinyumbani.

Upasuaji umebaini kuwa Wakise alikuwa na risasi mbili mwilini baada ya kujipiga kifuani huku mkewe akiwa na risasi saba ikiwemo shingoni na kichwani.

Wawili hao waliokuwa wanaishi kama bibi na bwana kuanzia mwaka 2012 walipofuzu kutoka chuo cha kutoa mafunzo ya Polisi cha Embakasi walikuwa wamefanikiwa kuwa na watoto wawili.