Diwani wa Mkomani kaunti ya Lamu Yahya Ahmed kwa jina maarufu Basode amehukumiwa kifungo cha miaka 13 na nusu na faini ya Sh800,000 kwa kupatwa na hatia ya kujaribu kuwaokoa wafungwa watatu wa ulanguzi wa dawa za kulevya.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu mkuu wa mahakama ya Lamu Allan Temba ameamuru kuwa makosa matatu ya kujaribu kuwaokoa watatu hao mwaka 2017 yanavutia kifungo cha miaka mitatu kila mmoja.

Kwenye shtaka la kwanza, diwani huyo pamoja na wenzake ambao hawakuwa mahakamani walijaribu kumuokoa ZamZam Mohamed Salim aliyekuwa amehukumiwa kifungo cha miaka Ishirini jela kwa kukutwa na hatia ya ulanguzi wa dawa za kulevya Juni, 2017.

Shtaka la pili linamuhusisha mwanasiasa huyo na kujaribu kumuokoa mfungwa Ali Mzee Ali aliyekuwa anahudumia kifungo cha miaka kumi kwa makosa ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Shtaka la tatu ni pale alijaribu kumuokoa mfungwa Nyathumani Yusuf aliyehukumiwa kifungo cha miaka mitano jela.