Muwaniaji wa chama cha ODM kwenye uchaguzi mdogo uliokamilika wa Matungu kaunti ya Kakamega David Were amewasilisha kesi mahakamani kupinga ushindi wa mwenzake wa chama cha Amani National Congress (ANC) Oscar Nabulindo.

Kwenye kesi yake, Were anadai kuwa maajenti wa chama cha ANC pamoja na maafisa wa tume ya uchaguzi IEBCwalihusika katika visa vya udanganyifu na kusababisha kushindwa kwake kwenye uchaguzi huo wa Machi 4.

Kupitia mawakili wake, mbunge huyo wa zamani anadai kuwa maafisa wa IEBC waliwanyima maajenti wake fursa kushuhudia ufunguzi wa masanduku yaliyokuwa na karatasi za kupigia kura sawa na kufuatilia shughuli nzima ya kupiga kura.

Ameongeza kuwa maajenti wake walifukuzwa katika kituo cha kuhesabia kura na kwamba wakati wa kuhesabu kura, baadhi ya fomu za 35A hazikutiwa saini na maajenti wa chama cha ODM.

Nabulindo alitangazwa mshindi na IEBC baada ya kupata kura 14,260 huku Were akipata kura 10,565.