Jumbe za matumaini zimetawala kheri njema kwa wakenya msimu huu wa pasaka ambao kwa mwaka wa pili mfululizo unaadhimishwa chini ya masharti makali kuzuia maambukizi ya virusi vya corona.
Katika ujumbe wake, Rais Uhuru Kenyatta amewataka wakenya kuwa na tumaini kuwa licha ya changamoto zinaozletwa na janga la corona, kuna tumaini katika Yesu.
Rais Kenyatta anasema kuwasili kwa chanjo ya corona kunatoa tumaini la kushinda vita dhidi ya janga hilo na kutaka kila mmoja wetu kutekeleza jukumu lake kwa kufuata masharti yaliyotolewa na wizara ya Afya.
Ujumbe sawia na huo umetolewa na Naibu Rais William Ruto ambaye ameelezea matumaini yake kuwa janga la covid19 ambalo limesabbaisha uchungu na mzigo mkubwa ulimwenguni litakwisha.
Katika ujumbe wake kwa wakenya, Dr Ruto amesema huu ni msimu wa kukumbuka machungu, kujitolea na kisha tumaini lililopo ndani ya Yesu.
Kwa upande wake aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga amewataka wakenya kuwa na imani kwamba miujiza aliyoifanya Yesu Kristo ikiwemo kufufuka baada ya siku tatu anaweza kuifanya hata leo.