Mlinzi mmoja anayedai kupigwa na aliyekuwa mbunge wa Tetu Ndung’u  Gethenji amemtaka Hakimu mkuu wa mahakama ya Milimani Martha Mutuku kujiondoa kwenye kesi  hiyo.

Godfrey Mutua wa kampuni ya ulinzi ya Securex kupitia kwa wakili wake Profesa George Wajackoyah amesema hajaridhishwa na vile hakimu Mutuku amekuwa akiiendesha kesi hiyo na kumtaka ajiondoe.

Hakimu Mutuku hata hivyo amesema mlalamishi hakuwa amewasilisha ombi hilo kirasmi mahakamani na kumtaka kufanya hivyo kabla ya kutoa mwelekeo tarehe 12 Aprili mwaka huu.

Mawakili wa Gethenji, wakiongozwa na Ishmael Nyaribo wamepinga ombi hilo wakidai mlalamishi hakuwa amewapa nakala ya barua waliyomwandikia Hakimu Mutuku kuelezea kutoridhishwa kwao na jinsi amekuwa akiendesha kesi hiyo.

Githenji alinaswa kwenye kamera za CCTV akimpiga mlinzi huyo katika lango la kampuni ya Kihingo Village tarehe tano mwezi Februari.