Vyama tanzu kwenye uliokuwa muungano wa upinzani NASA vimekasirikia kufukuzwa kwa seneta wa Kakamega Cleophas Malala kwenye wadhifa wa naibu kiongozi wa walio wachache katika bunge la Senate.

Chama cha Amani National Congress (ANC) kinachoongozwa na Musalia Mudavadi kimelaumu ODM kwa hatua hiyo kikisema hakitanyamaza.

Mudavadi ametaja hatua hiyo kama inayohujumu demokrasia huku akisema atasimama na Malala.

Naye kiongozi wa chama cha FORD K na seneta wa Bungoma Moses Wetangula ametaja kama ubinafsi na ukiukaji wa sheria kung’olewa kwa Malala akihusisha hilo na matokeo ya uchaguzi mdogo Matungu ambapo ANC walishinda.

Katika kikao cha maseneta wa muungano wa NASA kilichoongozwa na kiongozi wa wachache James Orengo, maseneta hao wamemtimua Malala kwa kile wanadai ni utovu wa nidhamu.

Nafasi yake imechukuliwa na seneta wa Kilifi Steward Madzayo.