Serikali imezionya hospitali dhidi ya kuitisha kiasi kikubwa cha pesa ili kuwakubali wagonjwa kulazwa katika vyumba vya wagonjwa mahututi (ICU).

Wizara ya afya kupitia katibu wake mkuu Dr. Rashid Aman inasema licha ya kwamba idadi ya wagonjwa wanaotafuta matibabu baada ya kuonesha dalili za ugonjwa wa corona inazidi kupanda, hospitali hazitaruhusiwa kuitisha kiasi kikubwa cha pesa kwani huo ni ukiukaji wa maadili.

Ameeleza kuwa tuko katikati ya janga la kimataifa na haistahili hospitali za umma na zile za kibinafsi kutumia nafasi kuwanyanyasa wanaotafuta matibabu kwa kuwapora pesa kama inavyoripotiwa.

Yanajiri haya wakati ambapo Kenya imeripoti maambukizi mapya 1,127 ya corona katika muda wa saa Ishirini na nne zilizopita baada ya kupima sampuli 5,393 na kufikisha idadi hiyo kuwa 123,167.

Dkt. Aman ametangaza maafa ya wagonjwa 25 zaidi na kufikisha idadi hiyo kuwa 2,048.

Idadi ya waliopona imefikia 90,586 baada ya kupona kwa watu 210 zaidi.