Rais Uhuru Kenyatta ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki amewaongoza wenzake kutoka barani Afrika kuhudhuria mazishi ya kitaifa ya rais wa Tanzania Hayati John Pombe Magufuli.

Katika hotuba yake, rais Kenyatta alimtaja hayati Magufuli kama kiongozi shupavu na aliyejali maendeleo ya Watanzania.

Marais wengine waliohudhuria hafla hiyo ya kumuaga Magufuli ni pamoja Mokgweetsi Masisi (Botswana), Cyril Ramaphosa (Afrika Kusini), Filipe Nyusi (Mozambique), Félix Tshisekedi (Congo), Lazarus Chakwera (Malawi), Emmerson Mnangagwa (Zimbabwe) miongoni mwa wengine.

Akisisitiza kwamba atawajibikia majukumu yake bila kuogopa, mrithi wa Magufuli rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemuomboleza marehemu akimtaja kama rais aliyejitahidi kuhakikisha kuwa rasilimali za umma zimetumika vyema.

Kulishuhudiwa na vilio na majonzi katika bunge la Tanzania wakati mwili wa marahemu Magufuli ulifikishwa kwa heshima za mwisho.

Mwili huo kisha ulisafirishwa kupitia barabara mbalimbali za jijini Dodoma, ukifuatwa nyuma na mamia ya waombolezaji.

Magufuli aliafriki Jumatano wiki iliyopita kutokana na mshtuko wa moyo.