Aliyekuwa rais wa Tanzania John Pombe Magufuli atazikwa Alhamisi ijayo ya tarehe 25 Machi ametangaza rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.

Kifo cha Magufuli kilitangazwa Jumatano Machi 17 kutokana na kile serikali ilitaja kama matatizo yanayoambana na moyo.

Kabla ya mazishi yake nyumbani kwake Chato, Watanzania katika maeneo mbali mbali ikiwemo Dodoma na Mwanza watapewa muda wa kuuaga mwili wa marehemu Magufuli aliyefariki kutokana na matatizo ya moyo.

Rais ametangaza kuwa mwili wa mwenda zake utaagwa Jumamosi Machi 20 na viongozi kabla ya wananchi kupewa fursa katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.

Magufuli alichaguliwa kwa mara ya kwanza 1995 katika nafasi ya ubunge, na akahudumu katika baraza la mawaziri katika nafasi ya naibu waziri wa ujenzi kuanzia 1995 hadi 2000.

Baadaye alihudumu kama waziri wa ujenzi kuanzia 2000 hadi 2006, waziri wa ardhi na maendeleo ya makaazi mwaka 2006 hadi 2008, na waziri wa ujenzi kwa mara ya pili kuanzia 2010 hadi 2015.

Akisimama kama mgombea wa chama tawala – Chama cha Mapinduzi CCM, Magufuli alishinda uchaguzi wa 2015 na aliapishwa Novemba 5, 2015.