Rais Uhuru Kenyatta ametangaza siku saba za maombolezo kufuatia kifo cha rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, 61.

Rais Kenyatta ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ameagiza bendera ya Kenya na zile za Afrika Mashariki kupandishwa nusu mlingoti kuanzia leo kwa heshima za mwendazake mpaka atakapozikwa.

Rais Kenyatta ameelezea kusikitishwa kwake na kifo cha rais Magufuli akisema alikuwa rafiki na kiongozi aliyejitolea kuimarisha maisha ya Watanzania.

Rais Kenyatta vile vile amesema amezungumza na Makamu wa rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa njia ya simu kutuma risala zake za rambirambi wa taifa la Tanzania.

Bi. Samia Suluhu Hassan ametangaza kuwa Dkt. Magufuli amefariki dunia katika hospitali ya Mzena iliyopo jijini Dar es Salam Jumatano mwendo wa saa kumi na mbili jioni saa za Afrika Mashariki kutokana na matatizo ya moyo.

Amesema kwamba rais Magufuli alianza kuugua mnamo tarehe 14 mwezi Machi na kulazwa katika hospitali hiyo ambapo alifariki.