Viongozi mbalimbali wanaendelea kutuma risala za rambirambi kwa familia ya rais John Pombe Magufuli na raia wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amemtaja Magufuli kama kiongozi aliyetia bidii katika kufanikisha ukuaji wa jumuiya ya Afrika Mashariki kiuchumi.

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amesema amesikitishwa na taarifa za kifo cha Magufuli akimtaja kama kama kiongozi aliyepigania maslahi ya watu wake.

Paul Kagame wa Rwanda amesema mchango wa Magufuli katika kanda hii hauwezi sahaulika kamwe. Amesema taifa la Rwanda linasimama na Tanzania wakati huu mgumu.

Naibu rais William Ruto amesema Magufuli anaacha nyuma uongozi ambao uko karibu na mwananchi kutokana na juhudi zake kutatua matatizo ya wananchi.

Kinara wa chama cha ODM Raila Odinga na mwenzake wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka wamemtaja Magufuli kama kiongozi aliyejaribu kuimarisha hali ya raia wa Tanzania.

Odinga amesema kwamba rais Magufuli amekuwa rafiki yake wa muda mrefu na kwamba amekuwa kando yake wakati mgumu alipomuhitaji.

Amesema kwamba tangazo la kifo chake amelipokea na huzuni kubwa akiongezea kwamba anasimama na familia ya marehemu wakati huu wa maombolezo.

Kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi amesema anasimama na Watanzania kipindi hiki kigumu cha msiba na kuomba kwamba katiba yao iwaongoze wakati huu wa mpito.

Baraza la magavana (CoG) pia limetuma risala za rambirambi kwa raia wa Tanzania kufuatia msiba huo.

Taifa la Marekani pamoja na waziri mkuu wa Uingereza Boris Johnson wameelezea kusikitishwa kwao na kifo hicho cha Magufuli. Boris Johnson amesema kwenye Twitter,’‘ Fikra zangu zipo na wapendwa wake pamoja na Watanzania’’.

Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright ametuma salamu za rambirambi kwa Watanzania kupitia ukurasa wake wa Twitter; “Kwa niaba ya watu wa Marekani, Ninatuma salamu zangu za rambirambi kwa kila mmoja anayeomboleza kifo cha Rais Magufuli.

Ifahamike kuwa Marekani iko pamoja na Watanzania katika wakati huu mgumu”.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la Afya Duniani (WHO) Tedros Adhanom ametuma risala za rambirambi kwa Watanzania na serikali ya nchi hiyo kufuatia kifo hicho. Kupitia ujumbe wa Twitter Tedros amesema Shirika hilo limewaweka kwa maombi Watanzania pamoja na familia ya rais Magufuli wakati huu mgumu.

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro, ametuma salamu za rambi rambi kwa Watu wa Tanzania kufuatia kifo cha Rais John Magufuli.

Taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya nje imesema “tunasimama” na “ndugu zetu wa Tanzania”.