Mtu na mkewe wameishtaki hospitali ya Nairobi South kwa kukwamilia wanao wawili wachanga kutokana na deni la Sh3.5M wanalodaiwa.

Charles Ndonye na mkewe Virginia Olembo walibarikiwa na watoto wanne waliozaliwa mwezi jana.

Kupitia kwa wakili wao Alex Mola, wawili hao wanasema walibarikiwa na watoto hao Februari 1 ila wakaruhusiwa kuondoka na watoto wawili pekee kwa sababu hawakuwa na pesa zote walizokuwa wanadaiwa.

Stakabadhi za mahakama zinaonesha kuwa hospitali hiyo iliwaambia kwamba watoto hao walikuwa wanaendelea kutibiwa lakini baadaye ikabadili msimamo na kusema wataruhusiwa kuwachukua iwapo watalipa bili wanayodaiwa.

Wazazi hao wanahoji kwamba kuendelea kuwazuilia watoto wao ni kinyume cha sheria na hatua hiyo inahujumu haki zao.

Wameongeza kuwa gharama hiyo ilongezeka kwa sababu watoto hao walizaliwa kabla ya muda wao na ilibidi wapewe matibabu zaidi.