Diwani wa wadi ya Muguga kaunti ya Kiambu Eliud Ngugi Ngige amefariki kutokana na matatizo yanayoambatana na corona.

Akidhibitisha taarifa hizo, spika wa bunge la kaunti ya Kiambu Stephen Ndichu amesema Ngugi alifariki katika hospitali ya chuo kikuu cha Kenyatta alipokuwa amelazwa.

Ndichu anasema Ngugi alianza kuwa mgonjwa wakati wakiwa kwenye kongamano moja kaunti ya Mombasa kabla ya kutibiwa na kuruhusiwa kurejea nyumbani.

Anasema alipofika nyumbani kwake, alizidiwa na maumivu na kupelekwa katika hospitali hiyo ya KU ambapo alilazwa kabla ya kufariki.

Ngugi aliwania kiti hicho cha Udiwani mwaka 2013 kupitia kwa chama cha Farmers lakini akashindwa kabla ya kuwania tena kupitia kwa chama cha Jubilee katika uchaguzi mkuu uliopita na kuibuka mshindi.

Atakumbukwa katika mchango wake wakati wa vikao vya kutimuliwa kwa aliyekuwa Gavana Ferdinand Waititu.