Makundi mbalimbali yamefika mbele ya bunge kutoa maoni yao kuhusu mswada wa marekebisho ya katiba BBI.

Muungano wa wanabodaboda nchini ukiongozwa na mwenyekiti wa kitaifa Kevin Mubadi umeunga mkono mswada huo ukisema kuwa kupitia kwa handisheki, amani na udhabiti vimerejea nchini na kuwawezesha kuendelea na shughuli za kujitafutia riziki.

Nayo mashirika yasiyo ya kiserikali yakiongozwa na mwenyekiti wao Stephen Cheboi yamesifia mapendekezo kwenye mswada huo ikiwemo kuongezwa kwa mgao wa pesa katika serikali za kaunti yakihoji kuwa itakuwa na manufaa.

Aidha makundi ya akina mama kutoka mashinani yamefika mbele ya kamati hiyo ya bunge la kitaifa na lile la Senate kuhusu haki na maswala ya kisheria chini ya uenyekiti wa seneta wa Nyamira Okongo Omogeni na mbunge wa Kangema Muturi Kigano kutoa maoni yao.

Hata hivyo chama cha Mawakili nchini LSK kupitia mwenyekiti wake Nelson Havi kimepinga mswada huo na kulitaka bunge kuukatalia mbali.

Mswada huo ulipitishwa na mabunge ya kaunti yapatayo 43, kukatiliwa na matatu huku bunge la Uasin Gishu likiwa la kipekee ambalo halikupiga kura ya kuunga mkono au kukataa.