Mahakama kuu ya Siaya imemhukumu kifungo cha siku moja jela mwanamke aliyepatikana na hatia ya kumuua mumewe aliyekuwa akimdhulumu.

Akitoa uamuzi huo, jaji Roselyne Aburili ameamuru kwamba mwanamke huyo Truphena Ndonga Aswani ambaye ameteswa sana alimuua mumewe ambaye siku hiyo alirejea nyumbani akiwa mlevi na mwenye hasira katika juhudi za kujilinda.

Jaji huyo ameamuru kwamba Ndonga anahitaji kupewa ushauri nasaha kutokana na yaliyomkumba kwa sababu amepitia hali ngumu ikiwemo kuchapwa na marehemu mumewe ambaye amemvumilia licha yake kuwa na virusi vya UKIMWI.

Kabla ya mauji hayo, mahakama imeambiwa kuwa mwanamke huyo wakati mmoja alilazwa hospitalini baada ya kupigwa na kuumizwa na marehemu mumewe wakati wa ugomvi.

Jaji Aburili ameongeza kuwa mshtakiwa hapaswi kupewa adhabu kali kwa sababu mbali na kumzalia marehemu mtoto mmoja, bado anawatunza watoto wa mume huyo ambaye mkewe awali alimuacha kutokana na mateso ya kinyumbani aliyokuwa anapitia.

Aidha, jaji Aburili amewahimiza wanawake kutoroka kwenye ndoa zilzojaa dhulma na kuripoti visa kama hivyo kwa asasi husika ili hatua zichukuliwe.