Mama na mwanawe wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumuibia mtoto mfanyikazi wa nyumbani kaunti ya Nairobi.

Mahakama imeambiwa kuwa Grace Akinyi na bintiye Nelly Achieng waliiba mtoto huyo kutoka kwa mamake tarehe moja mwezi huu katika bustani ya Uhuru katikati mwa jiji la Nairobi.

Wawili hao kisha walisafirisha mtoto huyo wa miezi minne hadi kaunti ya Bungoma na kumficha huko.

Hata hivyo wawili hao wamekanusha mashtaka dhidi yao mbele ya hakimu mkuu Martha Mutuku wa mahakama ya Milimani, na badala yake kusema walikutana na mama mtoto akitafuta kazi ya nyumbani.

Hakimu Mutuku ameagiza wawili hao wazuiliwe rumande Industrial Area hadi Machi 18 kuruhusu uchunguzi zaidi dhidi yao.

Akinyi na bintiye sasa wanajiunga na mumewe ambaye pia anazuiliwa kwa tuhuma kama hizo za wizi wa mtoto na ulanguzi wa watu.

Aidha, upande wa mashtaka umeiomba kuruhusiwa kuwasaifirisha washukiwa hao hadi katika mahakama ya Busia ambapo watafunguliwa mashtaka pamoja.