Wanasiasa sio miongoni mwa watu Milioni 1.25 watakaopewa chanjo ya corona kwenye awamu ya kwanza itakayotolewa kuanzia Ijumaa.

Badala yake waziri wa afya Mutahi Kagwe katika taarifa amesema zaidi ya wahudumu wa afya wapatao 400,000 kote nchini ndio watakaopewa kipau mbele pamoja na wafanyikazi wa umma wanaotoa huduma muhimu sambamba na ilivyokuwa imepangwa hapo awali.

Waziri Kagwe vile vile amedhibitisha kwamba amepokea chanjo hizo zilizowasili nchini akisema zitasambazwa katika hospitali zote za rufaa katika kaunti mbalimbali nchini.

Aidha, waziri Kagwe ametangaza kupatikana kwa visa vipya 331 vya corona baada ya kupima sampuli 4,725 na kufikisha idadi ya visa hivyo kuwa 106,801.

Watu wengine 54 wamepona ugonjwa huo na kufikisha idadi hiyo kuwa 86,914 huku maafa yakifikia 1,866 baada ya kufariki kwa wagonjwa 3 zaidi.